Kwa mujibu wa shirika la habari la kimataifa la AhlulBayt (A.S) -ABNA- Qudumi alieleza kuwa utawala wa Kizayuni, kwa msaada wa moja kwa moja kutoka Marekani, ulipanga shambulio hilo wakati wa kikao cha mashauriano cha viongozi wa Hamas huko Doha, lakini mpango huo haukufanikiwa.
Qudumi alisisitiza:
“Kama ilivyo desturi, serikali ya Marekani haizingatii ahadi zake na mara zote hujificha nyuma ya pazia la mazungumzo na mapendekezo ya kinafiki, hali inayotoa nafasi kwa utawala wa Kizayuni kutekeleza jinai zake. Safari hii, wakati uongozi wa Hamas ulikuwa unachambua kile kinachoitwa ‘mpango wa Marekani’, wavamizi haram wa kizayuni walishambulia makao ya harakati hiyo katika nchi ambayo ni moja ya wapatanishi muhimu - kwa uratibu na Marekani.”
Kwa mujibu wa Kituo cha Habari cha Palestina, Qudumi alithibitisha kuwa:
“Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, jaribio hilo la kigaidi na la kisaliti halikufanikiwa, na viongozi wa harakati ya Hamas walinusurika. Hata hivyo, baadhi ya ndugu zetu katika timu ya uendeshaji na wasaidizi waliuawa shahidi. Tunawaona kuwa ni mashahidi mbele ya Allah, na tunatoa rambirambi zetu pamoja na pongezi kwa familia na jamaa zao.”
Mwakilishi huyo wa Hamas nchini Iran pia aliilaumu jumuiya ya kimataifa pamoja na mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya utawala wa Kizayuni. Aliongeza:
“Tayari tumesisitiza mara nyingi kuwa adui Mzayuni hana nia yoyote ya kufikia makubaliano ya amani, na mwenendo wa serikali ya Marekani unaendelea kuutia moyo utawala huo wa kibaguzi kuendeleza mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Gaza.”
Katika hitimisho la kauli yake, Qudumi aliwahutubia wananchi jasiri wa Gaza kwa kusema:
“Uwanja huu wa vita kwa mara nyingine umeonyesha uso wa kweli wa utawala wa kigaidi na wa hadaa wa Kizayuni. Hakuna njia nyingine isipokuwa kujilinda. Tunaapa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya watu wa Palestina kuwa tutaendeleza njia hii hadi mwisho - ushindi au kufa shahidi.”
Your Comment